Hivi Kwanini Unaitwa Hivo..

TAMKA na ANDIKA  jina LAKO vizuri

Kila mtu hasa vijana wengi wana majina ya utani yaani "a.k.a..."kama vile platinum, Jamaica,Anyama,Master e,n.k

Mara nyingi haya tunapewa Na marafiki kutokana tabia zetu kwao au kufanania na mtu mwenye jina hilo..Wakati mwingine tunajibatiza wenyewe.


Lakini bado tunapozaliwa wazazi nao utupatia majina hasa
Kutokana Na hali,wakati Na hata majira ya mwaka  tulipokuwa tunazaliwa
Mfano "Hayo Malando,Shida,Sipendeki n.k
JINA umtambulisha mtu

Mfano. “Paulo mtumwa wa Kristo” (Rum 1:1-7) Saulo muuaji aliandika vizuri jina lake akawa Paulo mtumwa wa Yesu

Nukuu: “Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao” (Mathayo 1: 21). Yesu ameandika vizuri jina lake. Ni mwokozi na mkombozi.

Nukuu: “…‘Yozefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu..” (Mathayo 1: 18-20). Yosefu angemwacha Bikira Maria angeitwa Yosefu mvurugaji wa mpango wa Mungu. Aliandika jina lake vizuri ni Yozefu Baba Mlishi wa Yesu  Mlinzi wa Familia Takatifu

Watu wanachagua majina kutokana na tabia na fadhila za waliokuwa na majina hayo. Papa Fransisko  alichagua jina hilo kutona na tabia ya Mt. Fransisko wa Assisi. Papa Fransisko ambaye jina lake kabla ya kuwa papa aliitwa Jorge Mario Bergoglio alisema, “Nilipofikiria maskini nilifikiria Fransisko wa Assisi. Halafu nilifikiria vita vyote Fransisko ni mtu wa amani pia. Ndivyo jina Fransisko lilivyokuja moyoni mwangu: Fransisko wa Assisi kwangu ni mtu wa umaskini, mtu wa Amani, mtu anayependa na kulinda mazingira.” Kuna majina ambayo wazazi hawawapi  watoto wao kwa sababu waliyokuwa nayo hawakuyaandika vizuri, hawakuyatendea haki majina yao: mfano jina Kaini, Kaini alimuua ndugu yake Habili. Jina Yuda Iskarioti mzazi hampi mtoto wake. Kwa sababu Yuda Iskarioti alimuuza Yesu. Jina lina nguvu. Jina linapotajwa hisia fulani zinajitokeza. Jina linapotajwa kinachokumbukwa ni tabia ya mwenye jina, mwonekano wake, sifa zake, uzuri wake, ubaya wake, fadhila zake, vilema vyake, vionjo vyake. Kila unachowaza unaandika jina lako. Kila unachoota, unaandika jina lako. Kila unachosema unaandika jina lako. Kila unachotenda unaandika jina lako. Chunga mawazo yako yanageuka kuwa maneno. Chunga maneno yako yanageuka kuwa matendo. Chunga matendo yako yanageuka kuwa tabia. Chunga tabia yako inageuka kuwa desturi. Chunga desturi yako inageuka kuwa hatima yako. Kuna majina ya wanyama ukiyataja tabia zao zinakuja akilini: sungura-ujanja, kinyonga-ugeugeu, kondoo –upole, nyoka –ukatlli. Wanyama hawa ni kama wameandika majina yao vibaya.

Mojawapo kati ya majina yanayopendwa ni Yosefu. Maana ya jina hili ni Mungu anaongeza. Jina la utani la Yosefu ni Joe. Jina la kike ni Josephina. Katika Biblia lilikuwa jina la mtoto wa 12 wa Yakobo mtoto mpendwa. Yosefu wa Agano la Kale aliandika jina lake vizuri. Kwanza alikuwa mtu wa ndoto, maono na dira. Pili alikuwa shujaa wa usafi wa moyo yaani mwaminifu. Tatu alikuwa mtu wa subira. Nne alikuwa mtafsiri mzuri wa ndoto. Tano alikuwa msimamizi mzuri wa chakula. Sita hakulipiza kisasi kwa ndugu zake waliomuuza. Saba aliyatumia machozi kama tiba.  Alitembea na Mungu. Hivyo liandike vizuri jina lako kama Yosefu wa Agano la Kale.

Wazazi wa Yosefu Baba Mlishi wa Yesu walimpa mtoto wao jina hili Yosefu sababu liliandikwa vizuri. Yosefu Baba Mlishi wa Yesu aliliandika vizuri jina lake. Tunasoma hivi katika Biblia: “Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yosefu, mumwewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, ‘Yozefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu” (Mathayo 1: 18-20). “Mt. Yosefu alikuwa mtu wa haki, mfanyakazi asiyechoka, mlinzi mwadilifu wa wale waliowekwa katika uangalizi wake,” alisema Mt. Papa Yohane Paulo II. Aliandika jina lake vizuri kwa kuwa mtu wa haki, kuwa na wazo la kutomwaibisha Bikira Maria hadharani, mlinzi, pia jasiri. Malaika alimwambia hasiogope. Hofu ni adui mkubwa. Neno “usiogope” katika Biblia limerudiwa mara 365. 

Linapotajwa jina la Yosefu Baba Mlishi wa Yesu sifa za mwenye haki, mlinzi, mkimya zinajitokeza. Huyu aliandika vizuri jina lake. Limeandikwa kwenye mioyo yetu. Jina lako liandikwe kwenye mioyo ya watu. “Niliandika jina lako mawinguni, lakini upepo ulilipeperusha. Mtu Fulani alisema, “Niliandika jina lako kwenye mchango lakini mawimbi yalilisomba. Niliandika jina lako moyoni daima litabaki.”

Unaposikia jina Yesu wazo linalokuja akili mkombozi, mwokozi, alindika jina lake vizuri. Tunasoma katika Biblia, “Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao” (Mathayo 1: 21). Jina Yesu ni jina la Kigiriki linatokana na jina la Kiebrania “Yoshua,” maana yake “Mwenyezi Mungu ni Mwokozi.” “Yesu ni simba wa Yuda (Ufunuo 5:5) na Mwanakondoo wa Mungu (Ufunuo 5:6). Alikuwa na moyo wa simba na alikuwa kama mwanakondoo. Mwenye nguvu na mpole, mkali na mtaratibu, mshindani na mkubali wengine, jasiri na mwenye moyo uliovunjika. Anatuwekea mfano wa kuigwa,” alisema Yohane Piper. Yesu aliandika jina lake.

Kama uliandika jina lako vibaya liandike tena tunapojiandaa kumpokea Yesu Kristo katika mioyo yetu. Kuwa mkimywa kam Yozefu Baba Mlishi wa Yesu. Kuwa mwenye haki kama Yosefu. Usiwaaibishe wengine hadharani. Kuwa mlinzi wa wengine. Usiogope. Nguruwe alikuwa anazungumza na kuku na ng’ombe. Nguruwe alisema watu wanatumia jina la kuku vizuri na la ng’ombe vizuri, lakini jina langu wanalitumia kutukania wengine. Kuku alisema kuwa yeye anawapa binadamu mayai. Ng’ombe alisema, “Shida yako wewe nguruwe ukiwa hai hautoi. Mpaka ufe ndipo unatoa nyama.” Tutende mazuri tukiwa hai. Tutaandika majina yetu vizuri. 

#nkulanga.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Akili yako: Mafanikio yako: Umaskin mwiko

kazaliwa

Enemies is a kick to success